Dkt mpango: ecsa endeleeni kupambana dhidi ya magonjwa tishio.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango akiwahutubia Wanajumuiya wa Afya Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Jijini Arusha.

 Egidia Vedasto 

Arusha.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameitaka Jumuiya ya Afya kwa Nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA) kuendelea kupambana kufanya tafiti  zenye majibu juu ya magonjwa tishio yanayoambukizwa na yasiyoambukizwa.

Akizungumza katika mkutano wa maadhimisho ya miaka 50 ya Jumuiya ya ECSA, uliofanyika Jijini Arusha, wenye muungano wa Nchi (9) Tanzania, uganda, Kenya,  Eritrea, Botswana, Lesotho, Zimbabwe, Malawi na Muswatin, amesema Jumuiya hii ni muhimu kwa Waafrika katika kushughulikia masuala ya afya ambayo ndio msingi wa maisha.

Pia amesema, ni muhimu kuendelea kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambayo pia yanaathiri sekta ya afya kwa kusababisha mlipuko wa baadhi ya magonjwa kama malaria na shinikizo la damu.

“Kipekee nampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Dkt. Faustine Ndugulile kuwa mgombea nafasi ya  Mkurugenzi Mwakilishi wa Afya Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika ambaye naamini ataleta mageuzi makubwa” amesema Dkt. Mpango.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Jumuiya hii ya (ECSA) imeendelea kuleta mabadiliko chanya kwa sekta ya afya nchini ikiwa ni kutoa msaada kiufundi lakini pia kutoa udhamini kwa wataalam wa afya kuongeza elimu katika hospitali kubwa ili kuwa wabobezi katika magonjwa makubwa, masuala ya upasuaji, uuguzi na usingizi.

Waziri wa Afya nchini Tanzania Ummy Mwalimu.

“Nawakumbusha Watanzania kuacha matumizi holela ya dawa, kwani ni hatari na yanasabisha ugonjwa wa  usugu wa vimelea vya dawa dhidi ya magonjwa ambao ni tishio, hata mimi nauogopa, iwe kwa binadamu au mifugo  tumia dawa kwa maelekezo na ushauri wa  Daktari na hakikisha unamaliza dozi” amesisitiza Waziri Ummy.

Wanajumuiya kutoka nchi tisa za Kanda ya Afrika wakiwa katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 iliyofanyika leo jijini Arusha.

Hata hivyo, ameeleza namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri sekta ya afya, kwa kusababisha mlipuko wa magonjwa kwa maeneo ambayo hayakuwa na magonjwa hayo, kwa mfano Arusha na Lushoto kwa sasa kuna taarifa za uwepo wa malaria tofauti na hapo awali.

“Najivunia Tanzania kuwa makao makuu ya Jumuiya ya ECSA na maadhimisho ya miaka 50 kufanyika Jijini Arusha kwani wageni kutoka nchi tisa za Afrika wataongeza pato la  uchumi wa jiji hili na Taifa kwa ujumla” amesema Waziri Ummy.

Waziri anayeshughulikia masuala ya Afya nchini Uganda Dkt. Hanifa Kawoya amesema Jumuiya ya ECSA imeendelea kufanya vizuri na imeleta matokeo chanya katika masuala ya afya.

Waziri wa Afya wa nchini Uganda Dkt. Hanifa Kawoya akipokea tuzo kutoka kwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango.

“Tunaahidi kuendeleza ushirikiano katika jumuiya hii na kuwasihi nchi nyingine kujiunga ili kusukuma mbele utendaji na kushirikiana kimawazo na kushauriana juu ya mabadiliko ya tabia ya nchi na magonjwa ya mlipuko kama Ebola na COVID” amefafanua Dkt. Kawoya.

Dkt. Faustine Ndugulile (Mbunge) aliyependekezwa na Rais kuwa mgombea wa kiti cha Mkurugenzi Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani WHO Kanda ya Afrika, amesema iwapo atachaguliwa, ataimarisha mifumo ya afya Barani Afrika na kuhakikisha Waafrika wanapata afya bora, kwani Afya ni mtaji na ni mali.

“Naishukuru Serikali yangu  kuniamini na kuniteua kugombea nafasi hii, tayari  nimeungwa mkono na nchi za SADC na Afrika Mashariki, ambapo Shirika la Afya Duniani WHO lina kanda (6) na Kanda ya Afrika yenye nchi (42) ni miongoni mwake” ameeleza Dkt Ndugulile.