Na Seif Mangwangi, Arusha
KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii , imeupongeza Mfuko wa Jamii kwa Watumishi wa Umma(PSSSF) kwa uwekezaji wenye tija wanaoufanya katika miradi ya maendeleo na utoaji huduma bora kwa wanachama.
Akizungumza jana wakati wa ziara ya kamati hiyo, kwenye mradi wa Nyumba wa Olorien Njiro jijiji Arusha, Mwenyekiti wa kamati , Fatma Toufiq ameupongeza mfuko wa PSSSF, kwa ulipaji mafao kwa wakati kwa wanachama na kuondoa malalamiko kwa wanachama.

Amesema katika kuhakikisha PSSSF inapaa kiuchumi, imejenga vitega uchumi maeneo mbalimbali ikiwemo nyumba za makazi, hoteli na majengo ya kupangisha maofisi ikiwemo uwekezaji wa viwanja ili kuhakikisha mfuko huo unakusanya zaidi mapato.
“Tangu alipoingia Mkurugenzi wa PSSSF, Abdul -Razak Badru hadi sasa tunaona mafanikio lukuki, hata mradi huu wa Olorien ni kielelezo tosha cha kuhakikisha miradi yote inakuza mapato ikiwemo ulipaji wa mafao kwa wanachama sasa hivi husikii malalamiko pongezi kwa watendaji wote wa mfuko huu mnafanya kazi zinazoonekana kwa macho, “amesema

Aidha aliomba pia uwekezaji kama huo unaoleta tija kwa hafaka ufanyike na Dodoma ambako kuna uhitaji mkubwa wa makazi na Hoteli kutokana na shughuli za mkoa huo kuongezeka.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri MKuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema mfuko huo umejipanga kuhakikisha miradi yote inatekelezwa ikiwemo utoaji wa huduma bora kwa wanachama sanjari na ulipaji mafao kwa wakati.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF,Abdul Razzaq Badru amesema uhimilivu wa mfuko huo, upo vizuri na thamani ya mfuko imezidi kuongezeka huku wanachama wakiwa wanalipwa kwa wakati na miradi mingi ya mfuko huo ikiendeshwa kwa faida.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, tangu alipoingia madarakani amekuwa msaada mkubwa kuhakikisha mfuko huu unazidi kuimarika, aliposikia serikali inadaiwa akalazimika kulipa sehemu ya deni la Serikali kutoka Sh.Trioni 4.6 tulizokuwa tunadai hadi trilioni 2 ambazo na zenyewe zimeanza kumaliziwa taratibu,”amesema.
Amesema kutokana na kufanya vizuri, thamani ya mfuko huo inaongezeka na kukaribia trilioni 10 kiwango ambacho ni kikubwa na kinaendana na viwango vya kimataifa.
