Marekani, uingereza ‘waendelea kufuatilia’ kesi ya kabendera



Ofisi za ubalozi wa Marekani na Uingereza nchini Tanzania zimeendelea kumulika kesi ya mwanahabari maarufu wa uchunguzi nchini Tanzania, Erick Kabendera.

Wiki mbili zilizopita ofisi hizo zilitoa tamko la pamoja juu ya kuhusu kile walichokiita “wasiwasi wa kuzorota kwa kwa haki za kisheria nchini Tanzania.”

Katika tamko hilo, ofisi hizo mbili za ubalozi zinadai kuwa imedhihirika kwa zaidi ya mara moja watu kutiwa kizuizini kwa muda nchini Tanzania bila kupelekwa mahakamani na kubadilishiwa mashitaka na mamlaka zake za kisheria.

“Tuna wasiwasi hasa kwa tukio la hivi karibuni — jinsi ambavyo halikushughulikiwa kwa haki la kukamatwa, kuwekwa kizuizini na tuhuma za mashtaka ya mwandishi wa habari za uchunguzi Bw Erick Kabendera, ikizingatiwa ukweli kwamba alinyimwa haki ya kuwa na mwanasheria kwenye hatua za awali na kutiwa kizuizini kwake, ambapo ni kinyume cha sheria ya makosa ya jinai,” inasema sehemu ya tamko hilo.

Jumatano jioni, ofisi hizo mbili tena kwa kupitia mitandao ya kijamii zilitoa ujumbe kuwa wanaendelea kufuatili kesi ya Kabendera.

“Tunaendelea kufuatilia kesi ya Erick Kabendera. Haki za kisheria ni haki ya raia wot, na kuhakikisha upatikatnaji wa haki hiyo ni wajibu wa serikali zote,” unaeleza ujumbe ambao umechapishwa katika kurasa za twitter za Ubalozi wa Marekani na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi Sarah Cooke.