Meya wa arusha kupitia chadema kalisti lazaro ajiunga na ccm

Wakati
kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zikiendelea nchini, aliyekuwa
Meya wa Jiji la Arusha Kalisti Lazaro amejiunga na Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na kupokelewa na Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM.




Ndugu
Kalisti Lazaro aliyefika katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM
Lumumba jijini Dar es Salaam ameeleza amefikia uamuzi huo baada ya
kupitia wakati mgumu akiwa katika Wadhifa wake wa Meya wa Jiji la
Arusha.
Ndugu
Kalisti amesema amepokea barua za maonyo mara kadhaa kutoka Uongozi wa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambazo zilimtaka kutokutoa
ushirikiano na Viongozi wa Serikali ambao anatakiwa kufanya nao kazi
ngazi ya Mkoa na Wilaya na kutompongeza hadharani Ndg. John Pombe Joseph
Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambayo
ameifanya Nchini ikiwamo katika Mkoa wa Arusha.
Vitisho
vya mara kwa mara ikiwamo dhidi ya uhai wake ndio vimepelekea kujivua
nafasi zake zote katika Chadema na kujiunga na CCM, Chama ambacho
kinashughulika na utatuzi wa kero za wananchi. 

Ndg.
Lazaro pia amechukizwa na Chama chake kujitoa katika uchaguzi huku
akiita kitendo hicho uvunjaji wa demokrasia ambacho ndani ya masaa
mawili uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema iliwanyima mamilioni ya wapenda
demokrasia haki ya kushiriki katika Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa,
Vijiji na Vitongoji.
Ndg.
Kalisti Lazaro amesema sasa yuko tayari kuchapa kazi ya wananchi akiwa
ndani ya Chama ya Mapinduzi na kwamba yuko tayari kwa maelekezo ya kazi
kutoka Uongozi wa CCM.
Ndg.
Kalisti kwa kujiunga na CCM amejiuzuru nafasi ya Udiwani, Umeya wa Jiji
la Arusha, Uenyekiti wa Mameya na Madiwani wote wa Chadema Nchini na
Ujumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Ndugu Kalisti Lazaro atapokelewa rasmi na wanachama wa CCM Mkoa wa Arusha katika tarehe itakayopangwa hivi karibuni.
Imetolewa na,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)