Rais magufuli amtumbua mkuu takukuru

Rais Magufuli amemtumbua Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Mtwara, Stephen Mafipa kutokana na kukosekana
kwake katika mkutano wa hadhara alioufanya katika Kijiji cha Chukuku
kilichopo Masasi mkoani humo.


Akiwa Chukuku, wananchi walimueleza Rais kuhusu madai yao dhidi ya fedha wanazowadai vingozi wa chama cha msingi Amcos baada ya viongozi hao kutoweka na fedha hizo.


Baada ya kupata malalamiko hayo, Rais Magufuli alimuita Kamanda wa
Polisi wa mkoa ambaye alieleza kuwa wanaendelea kuwatafuta watuhumiwa.

Jibu hilo lilionekana kutomfurahisha Rais Magufuli ndipo alipotoa siku
tano kwa kamanda huyo kuhakikisha viongozi hao wanakamatwa na kufikishwa
kwenye vyombo vya sharia.

“RPC nakupa ndani ya siku tano waliokula fedha za wananchi wa hapa
wakamatwe na wapelekwe mahakamani, mshirikiane na Takukuru, kamanda wa
Takukuru mkoa yuko wapi,” aliuliza Rais Magufuli bila kupata majibu

Kufuatia ukimya huo aliomba simu yake kutoka kwa wasaidizi wake ambapo
alipewa na kumpigia Brigedia Jenerali Mbungo na kumuelekeza kumuondoa
kamanda huyo wa mkoa na kumtaka ampeleke mtu mwingine kwa ajili ya
kufanya kazi hiyo.

“Brigedia Jenerali, nipo hapa Masasai, nimemuita Kamanda wako wa
TAKUKURU hapa hayupo, nimemfuta kazi hapahapa. Sasa nakuagiza leo hii
uteue Kamanda mwingine, aje hapa asaidizane na RPC kuwakamata hao wezi
na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria.

“Hatuwezi tukavumilia huu ujinga na siwezi kukubali wananchi wangu
wakanyanyasika. nataka utekeleze mara moja,” alisema Magufuli wakati
akitoa maelekezo hayo kwa Brigedia Jen. Mbungo kupitia njia ya simu ya
mkononi.