Ruwasa mkoa wa shinyanga wapongezwa kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maji wilaya ya kishapu

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mbunge wa viti maalum kupitia CCM Mkoa wa Shinyanga Mhe.
Santiel Kirumba leo Jumatano Novemba 29,2023 amefanya ziara ya Wilaya ya
Kishapu kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa na wakala wa usambazaji maji
na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga.

Katika ziara hiyo Mhe. Kirumba ameambatana na viongozi
wa umoja wa wanawake wa chama cha mapinduzi UWT Mkoa wa Shinyanga wakiwemo
viongozi wa UWT kutoka kwenye Halmashauri zote sita za Mkoa wa Shinyanga.

Viongozi hao wametembelea  ujenzi wa mradi wa maji ya ziwa Viktoria
Seseko – Ngundangali unaotekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu kupitia mradi wa
P4R mradi huo unatekelezwa kwa muda wa mwaka  mmoja na 
unatarajiwa   kukamilika  Mwezi Machi,  2024.

Akisoma taarifa fupi ya mradi huo wa maji ya Ziwa Viktoria Seseko –
Ngundangali, meneja wa RUWASA Wilaya ya Kishapu mhandisi Dickson Kamazima amesema
mradi huo utawanufaisha wananchi katika vijiji vitano vya kata ya uchunga
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.

Katika ziara hiyo pia wametembelea ujenzi wa mradi wa
maji kata ya Igaga ambao thamani yake ni shilingi Bilioni 6.6 na kwamba mradi
huo utawanufaisha wananchi wa vijiji 13.

Baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu
wamesema kukamilika wa miradi ya Maji inayotekelezwa na wakala wa usambazaji
maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga itasaidia kumaliza
changamoto wanazokutana   nazo.

Wamesema wamekuwa wakitumia Maji ambayo si salama hali
inayohatarisha usalama wa Afya zao na kwamba ubali mrefu wa maji unasababisha migogoro
kwenye familia ikiwemo ukatili wa kijinsia ambapo wameishukuru serikali kupitia
RUWASA Mkoa wa Shinyanga kwa kurahisisha upatikanaji wa maji safi na salama.

Mbunge wa viti maalum kupitia CCM Mkoa wa Shinyanga Mhe.
Santiel Kirumba ameipongeza RUWASA Mkoa wa Shinyanga kwa kasi nzuri ya
utekelezaji wa Miradi huku akiwaomba wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali
ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuendelea
kutatua changamoto zilizopo.

 Mbunge wa Jimbo
la Kishapu Mhe. Boniphance Butondo amesema miradi ya maji inayotekelezwa na
RUWASA Mkoa wa Shinyanga katika jimbo hilo baada ya kukamilika upatikaji wa
maji utakuwa zaidi ya asilimia 65 na kwamba amewapongeza viongozi wa RUWASA
Mkoa wa Shinyanga kwa utekelezaji mzuri wa miradi hiyo.

Kwa upande wake meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga
Mhandisi Julieth Payovela ameeleza kuwa miradi yote ya Maji inayotekelezwa na
RUWASA Mkoani Shinyanga itakamilika kwa wakati pamoja na kuwapa vipaumbele wananchi
wazawa kwenye suala la ajira.

Mbunge wa viti maalum kupitia CCM Mkoa wa Shinyanga Mhe.
Santiel Kirumba na meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Julieth Payovela
upande wa kulia baada ya kuwasili katika kata ya Uchunga kwa ajili ya
kutembelea mradi wa maji leo Jumatano Novemba 29,2023.