Serikali yazindua mwongozo wa matibabu ya saratani nchini

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Serikali
ya Tanzania imezindua mwongozo wa kitaifa wa tiba ya magonjwa ya
saratani utakaoziwezesha hospitali za serikali na binafsi katika kutoa
matibabu kwa usawa na kurahisisha mawasiliano kati ya madaktari bingwa
na wataalamu wengine.


Kuzinduliwa
kwa mwongozo huo kumefuatia baada ya hospitali za kanda kuanza kutoa
tiba za saratani, kuongezeka kwa hospitali binafsi na za umma zinazotibu
ugonjwa huo kwa sasa nchini, huku kwa kipindi kirefu hospitali nyingi
zikitumia miongozo tofauti na ile ya nje ya nchi.

Akizindua
mwongozo huo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema huduma za saratani
zinasambaa katika hospitali mbalimbali nchini kwa sasa hivyo utoaji wa
huduma lazima uangaliwe ili zitoke kwa kiwango kinachopaswa.

Amesema
kuwepo kwa miongozo tofauti ilisababisha kutokuwepo kwa usawa katika
tiba za wagonjwa lakini pia kulikuwa na changamoto ya mgonjwa kuendelea
na tiba sahihi pindi akipewa rufaa kwenda hospitali nyingine.

“Kuwepo
kwa mwongozo huu kutawezesha kurahisisha mawasiliano kati ya madaktari
bingwa na wataalamu wengine wa matibabu ya saratani kote nchini,

“Kurahisisha
uandaaji wa maoteo na ununuzi wa dawa na vitendanishi vinavyotumika
katika matibabu ya saratani, mwongozo huu pia umetoa orodha ya dawa na
vifaa tiba kwa ajili ya matibabu ya saratani ambayo itatumika kama
mwongozo kwa ajili ya manunuzi na matumizi nchini,” amesema Ummy
Mwalimu.

Amesema
mwongozo huo pia itawezesha wananchi kupata huduma bora na za viwango
vya juu katika vituo vyote vya matibabu kwa kuwa tiba zote zitapangwa
kwa kufuata mwongozo huo.

Waziri
Ummy amesema pia utawezesha kutoa mwongozo kwa mfuko wa taifa wa bima
ya afya NHIF kuhusu dawa na vipimo mbalimbali stahiki kwa wagonjwa wa
saratani.

“Mfuko
wa Taifa NHIF uhakikishe unatumia mwongozo huu katika kuweka vitita vya
huduma za saratani hapa nchini kwani katika ile standard treatment
guideline kuna baadhi ya dawa za kutibu saratani hazikuorodheshwa, na
niwaambie mmeweka masharti magumu sana katika vipimo hivi CT Scan na MRI
nani anapima mara kwa mara tuondoe baadhi ya vikwazo na hili NHIF
mkalitekeleze,” ameagiza.

Ameagiza mwongozo huo utumike na vituo vyote vinavyotoa tiba za saratani nchini;
“Ninafahamu
hospitali zote zilishiriki kuuandaa hivyo sitegemei kusikia kuna
hospitali inafanya tiba nje ya mwongozo huu, ninaagiza pia wizara
kufanya mapitio ili kuhakikisha dawa zote zinazotibu saratani
zinakumuishwa katika mwongozo huu.”

Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dk Julius Mwaiselage
amesema, “Matumizi ya mwongozo huu yamefanyiwa majaribio kwa kipindi cha
miezi sita katika taasisi hii kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha St
Francisco.”