Tbs na taffa yakaa kujadili mipango kazi

Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora (TBS)
Bw.Mosses Mbambe (katikati) akifuatiliakikao kazi na Chama cha Mawakala
wa Forodha (TAFFA) kilichofanyika leo katika ofisi za Makao makuu TBS
leo Jijini Dar es Salaam.

Mawakala wa wa Forodha (TAFFA)
wakifuatilia kikao kazi ambacho kiliwakutanisha na Shirika la Viwango
Tanzania (TBS) Kujadili ni namna gani wanaweza kutatua changamoto zao
katika utendaji kazi wao.

NA EMMANUEL MBATILO

Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
wamekutana na wanachama wa chama cha Mawakala wa Forodha (TAFFA)
kwaajili ya kujadili ni namna gani wanaweza kuboresha utendaji kazi wao
katika kuhakikisha wanakuza biashara na kumlinda mtumiaji.

lengo ni kuwapitisha katika taratibu za
ukaguzi na upimaji wa bidhaa ambao unafanya na shirika hilo na vilevile
wamewapitisha katika mfumo wa electronic window system ili waufahamu
namna ya kuutumia na kurahisisha utoaji wa mizigo katika vituo vya
forodha.

Akizungumza mara baada ya mkutano huo
Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora (TBS) Bw.Mosses Mbambe amesema kuwa
changamoto iliyopo kwasasa ni utumiaji wa mfumo wa electronic window
system inaonekana kwamba baadhi ya mawakala hawaufahamu mfumo huo na
kuweza kupelekea ucheleweshaji wa utoaji wa mizigo kutoka katika vituo
vya forodha.

“Kama hauwezi kutumia huu mfumo kuna
athari zinaweza kujitokeza hasa kuchelewesha mzigo kutoka katika kituo
cha forodha na mzigo ukichelewa kutoka ina maana mteja hataweza kupata
mzigo wake kwa wakati vilevile inaweza kupelekea mlundikano wa mizigo
katika vituo vya forodha”. Amesema Bw.Mbambe.

Kwa upande wake Meneja wa masuala ya
ukaguzi wa bidhaa zinazotoka nje (TBS) Mhandisi Saidi Mkwawa amesema
kuwa kuna baadhi ya mawakala wamekuwa wakilalamika kuna tatizo kwenye
mfumo wa kuweza kufanya usajili na kuweza kutoa nyaraka zao kwaajili ya
kufanyiwa ukaguzi ambapo kumekuwa na changamoto mbalimbali.

“Dhamira ya Serikali ni kumuepushia
usumbufu yule wakala ambaye anafanya biashara kwasababu mfumo huu zamani
kila unaemuona wakala wa forodha alikuwa lazima aweze kufanya maombi ya
mifumo mbalimbali, aende Shirika la wakala wa meli TASAC, afike TBS
kwenye mfumo tofauti ama aende kwenye mifumo mingine ya serikali. Lakini
serikali ikaona yakwamba kuwe na mfumo mmoja ambao utarahisisha na
kutoa ufanisi lakini kila jambo jipya linalokuja lazima liwe na
changamoto zake”. Amesema Mhandisi Mkwawa.

Nae Katibu Mtendaji (TAFFA) Bw.Elitunu
Mallamia amesema kuwa kupitia mkutano huo unazidi kukuza mahusiano yao
na TBS ambao wanashirikiana nao kwenye kusaidia nchi iweze kuingiza
bidhaa bora na bidhaa ambazo zitawalinda watumiaji.

Sambamba na hayo Mkuu wa Kitengo cha
Mahusiano na Masoko (TBS), Bi.Gladness Kaseka amewakaribisha wadau
mbalimbali wanaoona kuna changamoto wanazipitia katika utendaji ili
waweze kufanya nao kikao na kujadili ni namna gani wanaweza kumaliza ama
kupungua changamoto hizo.