Tcu yafanya uhakiki na utambuzi wa vyeti 8328 vya wahitimu wa vyuo vya nje

Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
TUME
ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) katika kipindi cha mwezi Novemba 2015 hadi
Novemba 2019 imefanya uhakiki na utambuzi wa uhalali wa vyeti 8328 vya
wahitimu waliotunukiwa tuzo zao na vyuo vikuu vilivyo nje ya Tanzania.


Akizungumza
katika mkutano na waandishi wa vyombo vya habari leo Jumanne (Januari
28, 2020) Jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles
Kihampa alisema kutokana na kuimarika kwa  mifumo ya kieletroniki, TCU
imefanikiwa kupunguza muda wa  uhakiki na utambuzi wa vyeti hivyo kutoka
siku 14 za awali hadi siku tatu.

Prof.
Kihampa alisema TCU imeimairisha mifumo yake ya kielektroniki ambayo
imeongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa kuboresha huduma inazotoa kwa
wateja na wadau wake kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Huduma kwa
wateja.

‘’Katika
kipindi hiki, zaidi ya maombi 1,077 ya hati ya kutokuwa na pingamizi
kwa wanaotaka kwenda kusoma elimu ya juu nje ya nchi, yamewasilishwa TCU
na kushughulikiwa na mfumo huu ni muhimu kwani unawapa fursa wananchi
kufahamu uhalali wa programu wanazokwenda kusoma, hivyo kuwaepusha
kupoteza rasilimali fedha za kusoma katika vyuo visivyotambulika’’
alisema Prof. Kihampa.

Aidha
Prof. Kihampa alisema kupitia miongozo yake TCU imeweza kusajili Wakala
tatu zinazodahili wanafunzi wanaotaka kusoma elimu ya juu nje ya
Tanzania, na kuzitaja wakala hizo ni pamoja na Global Education Link
Ltd, DARWIN Education Agency Ltd na Yahoma Educational Ltd, pamoja na
kupokea maombi ya wakala nyingine 7 zinazosubiri  taratibu za usajili.

Prof.
Kihampa alisema kwa mujibu muongozo huo, wakala wote hutakiwa kuwa na
mikataba maalum baina yao na vyuo vilivyopo nje pamoja na Cheti maalum
(NOC), na hivyo kuwataka wakala wote waliokidhi vigezo hivyo kutuma
maombi yao TCU na kukamilisha usajili kwa wakati.

Katika
hatua, nyingine Prof. Kihampa alisema katika kusimamia ubora wa elimu
inayotolewa na vyuo vikuu nchini, kati ya kipindi cha mwezi Oktoba 2016
hadi Januari 2017, TCU  ilifanya ukaguzi maalum wa kitaaluma kwa taasisi
64 za vyuo vikuu, vyuo vikuu vishiriki na vituo vya vyuo vikuu ili
kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi viwango vya kitaifa, kikanda na
kimataifa.

‘’Matokeo
ya ukaguzi yalibainisha kasoro mbalimbali katika uendeshaji wa vyuo
vikuu nchini, vyuo 45 vilikutwa na kasoro ndogondogo, vilipewa ushauri
na viliweza kurekebisha katika kipindi kifupi vikaendelea na utoaji wa
elimu ya juu na vyuo 19 vilikutwa na kasoro kubwa, vilipewa ushauri na
muda wa mrekebisho’’ alisema Prof. Kihampa.

Kwa
mujibu wa Prof. Kihampa alisema hadi sasa vyuo vikuu 9 kati ya 19
vilivyositishwa udahili vimefanya marekebisho makubwa na vimeruhusiwa
kudahili na kuendelea kutoa mafunzo kwa baadhi ya programu za masomo, na
kuvitaja vyuo hivyo kuwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Umoja wa Afrika
Tanzania (UAUT), Chuo Kikuu cha Teofila Kisanji (TEKU), Chuo Kikuu
Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora (AMUCTA), Chuo Kikuu Kishirishi
cha Marian (MARUCo).

Anavitaja
vyuo vingine ni Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala Nchini Tanzania
(KIUT), Chuo Kikuu Kishiriki cha Kikristo cha Tiba Kilimanjaro (KCMUCo),
Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stephano- Moshi (SMMUCo) na Chuo
Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Mt. Fransisko
(SFUCHAS).

Anaongeza
kuwa mifumo ya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara imefanya vyuo
kufanya maboresho makubwa katika miundombinu ya kufundisha na kujifunzia
ikiwa na pamoja na ujenzi wa maabara za kisasa, mifumo ya mawasiliano
ya kielektroniki, madarasa na kuongeza idadi ya viongozi na wahadhiri
wenye sifa.