Tfra yamkera waziri hasunga, ataka bei ya mbolea ishuke

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo, Songwe
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa
Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha kuwa inapanga na kusimamia bei
elekezi za mbolea kwa lengo la kumuwezesha mkulima kupata mbolea kwa bei
nafuu.


Amesema
kuwa bei ya sasa ya mbolea ya kukuzia na kupandia bado sio rafiki kwa
wakulima hivyo TFRA wana wajibu wa kuhakikisha kuwa bei inapungua Zaidi.

Waziri
Hasunga ameyasema hayo tarehe 21 Januari 2020 wakati wa ufunguzi wa
kikao kazi cha vyama vya ushirika kuhusu ununuzi wa mbolea kwa pamoja
(BPS) kilichofanyika katika ukumbi wa Mpendejirani eneo la Vwawa Mkoani
Songwe.

Amesema
kuwa Kanuni za usimamizi na uagizaji wa mbolea kwa pamoja zilitungwa
kufuatia tafiti za kina zilizofanywa na Watafiti wa ndani ya Nchi na
wengine kutoka Taasisi za Kimataifa ambapo Matokeo ya Tafiti hizo
yalionesha kuwa BPS inaweza kupunguza gharama ya uagizaji wa mbolea kwa
zaidi ya asilimia 50.

Lakini
pamoja na matarajio hayo ya serikali na wakulima nchini bado gharama za
mbolea sio rafiki kwa wakulima pamoja na bei kushuka mwaka 2019
ukilinganisha na miaka iliopita.

Pamoja
na Serikali kusisitiza wakulima kuvitumia Vyama vya Ushirika katika
utatuzi wa changamoto za kiuchumi na Kijamii, bado wanaushirika
wameshindwa kubuni mfumo madhubuti wa kuwaunganisha katika ununuzi wa
Pembejeo ambazo zingewapa unafuu wa gharama za uzalishaji pamoja na
kwamba Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002, kusisitiza kwamba
Ushirika ni chombo pekee cha kumletea mwananchi mnyonge maendeleo ya
kiuchumi na kijamii.

Waziri
Hasunga amewaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa Tayari Wizara ya
Kilimo kupitia kwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania imetoa Waraka
wa kuagiza Vyama vyote vya Ushirika kupeleka mahitaji yao ya mbolea
kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ili iagizwe kwa
pamoja kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS – Bulk
Procurement System).

Endapo
Vyama vya Ushirika vitaagiza mbolea kupitia BPS kwa kutumia dhamana za
Benki (Bank guarantees) zenye tozo ndogo (asilimia 1 – 4) na kusafirisha
mbolea kwa pamoja kwa njia ya reli, gharama zitapungua na mbolea ya NPK
itakuwa na bei ndogo kuliko DAP.

Amesema
Vyama vya ushirika vinapaswa kuwa ndio kimbilio la wakulima na hivyo
kuagiza mbolea kwa pamoja itapelekea kupungua kwa gharama za mbolea na
ziweze kufika kwa wakati.

Kadhalika,
katika mkutano huo Waziri Hasunga ameiagiza Taasisi ya Utafiti na
udhibiti wa Viuatilifu katika ukanda wa kitropiki TPRI kutoa mafunzo kwa
wananchi nchini kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu.

Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mhe John Palingo akimuwakilisha
mkuu wa mkoa wa Songwe katika mkutano huo ameipongeza serikali kwa
kuanzisha na kuvisimamia vyama vya ushirika nchini kwani kupitia umoja
huo wakulima wameendelea kunufaika ikiwa ni pamoja na kuwa na bei nzuri
ya mazao.

Amesema
kuwa pamoja na mambo mengine lakini pia ushirikuwa mkombozi kwa
wakulima kwani unawasaidiia wakulima kupata tija ya mazao na kuimarisha
kipato chao.

MWISHO