Na Zulfa Mfinanga, Manyara.
Hapo awali mwanzoni mwa miaka 2000 baadhi ya wanawake wanaoishi kata ya Nkaiti iliyopo wilaya ya Babati mkoani Manyara walitumika na majangili wa wanyamapori kama moja ya njia ya kuu ya usambazaji wa nyamapori mtaani.
Katika mbinu zao, majangili hao waliokuwa wanafanya ujangili katika hifadhi za wanyamapori za jirani na ushoroba wa Kwakuchinja, walikuwa wanawauzia Mama lishe katika maeneo ya vijiji hivyo hususan nyakati za minada kwa kuwa kundi hilo lina uhitaji mkubwa wa nyama hiyo haramu.
Kata ya Nkaiti yenye vijiji vinne vya Minjingu, Olasiti, Kakoi na Vilima vitatu ni miongoni mwa maeneo yanayopatikana ndani ya ushoroba wa Kwakuchinja. Ushoroba huo, unaopatikana katika mikoa ya Arusha na Manyara, ni mapitio na makazi ya asili ya wanyamapori yanayounganisha hifadhi mbili za Taifa za Tarangire na Ziwa Manyara.
Kwa mujibu wa wataalamu wa uhifadhi, Kwakuchinja ni miongoni mwa shoroba 20 nchini zilizopo hatarini kupotea kati ya 60 kutokana na tatizo la ujangili wa wanyamapori na ongezeko la shughuli za kibinadamu kama kilimo, ufugaji na ujenzi wa makazi.
Hata hivyo, kuanzishwa kwa Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori (Burunge WMA) mwaka 2006 ilianza kuwa mwanzo wa kukabiliana na ujangili katika ushoroba wa Kwakuchinja kupitia doria na shughuli nyingine za uhifadhi, kazi inayofanyika mpaka sasa.
Pamoja na jitihada hizo bado kuna baadhi ya majangili miaka ya hivi karibuni waliendelea kupenyeza nyama hizo mtaani kupitia minada katika maeneo hayo, jambo lililoifanya serikali na wadau kuongeza wigo wa kukabiliana nayo ili kuwalinda wanyamapori.
Kiongozi wa operesheni ya kudhibiti ujangili na uhifadhi maliasili katika ushoroba wa Kwakuchinja kutoka Taasisi ya Chem chem Association (CCA) Hamis Chamkulu anasema nyamapori huuzwa kwa makadirio ambapo pande moja lenye ukubwa wa kilo moja hadi kilo moja na nusu huuzwa kati ya shilingi 2,000 hadi 3,000.
Anasema bei hiyo iliwavutia zaidi wanunuzi ikilinganishwa na bei ya nyama ya ng’ombe, mbuzi au kondoo ambayo huuzwa kati ya shilingi 8,000 hadi 9,000 kwa kilo moja.
Mama ntilie watumika kuuza nyamapori mnadani
Baadhi ya wanawake wakazi wa vijiji hivyo wanasema kipindi hicho biashara ya nyamapori ilikuwa ikifanyika hadharani bila kificho hadi minadani na hakuna aliyefikiri ipo siku biashara hiyo itakuwa haramu pale ambapo muuzaji hatafuata sheria kuipata ikiwemo kupata kibali maalum.
Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009 imeweka bayana kuwa wanyama pori ni sehemu ya nyara za Serikali, hivyo mtu anayetaka kutumia wanyamapori ni lazima afuate taratibu za kisheria.
Licha ya kuanzishwa kwa sheria hiyo lakini bado uthibiti wa ujangili ulikuwa mgumu katika eneo hilo la ushoroba kutokana na kukosekana na chombo mahususi cha kusimamia sheria hiyo.
Tabia Daud (53) mkazi wa Mdori katika kijiji cha Vilima vitatu anasema kabla ya kuanzishwa kwa Burunge WMA wakazi wa eneo hilo walikuwa wanauza nyamapori hadharani na hakukuwa na woga wowote. .
“Nakumbuka hadi miaka ya 2000 bado tulikuwa tunauza na kula nyamapori bila wasiwasi, lakini siku zinazoendelea kusonga naona sheria zinazidi kuwa kali sana, sasa hivi ukikamatwa na nyamapori ujue utaozea jela, ulinzi ni mkali sana yaani siyo usiku wala mchana huwezi kukwepa ni lazima utakamatwa tu,” anasema Tabia akibainisha kuwa wakati huo majangili walikuwa wanauza zaidi nyama ya swala.
Tabia anakiri kuwahi kufanya biashara ya kuuza nyamapori kupitia biashara yake ya mamalishe katika minada ya Minjingu na Mwada na hata wateja wake walikuwa akifahamu kuwa wanakula nyamapori.
Majangili walikuwa na oda
Anasema alikuwa anapata nyama hiyo kutoka kwa wawindaji ambao kabla ya kwenda kuwinda walikuwa wanapita kwa wanunuzi (akiwemo yeye) na kuchukua oda ili wajue kiwango kinachotakiwa wakati wa kuwinda.
Anasema licha ya kuzaliwa jamii ya kimaasai ambayo haipendi kula nyamapori lakini baada ya kuolewa na kabila nyingine alikuwa akiila na kuuza nyama hiyo japo baadaye alilizimika kuacha kuuza kutokana na ugumu wa upatikanaji wake na adhabu kali kwa wanaokutwa na hatia ya ujangili tofauti na hapo awali.
Utoaji wa elimu unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi ikiwemo Chemchem Association na uimarishaji doria umepunguza kwa kiwango kikubwa uwindaji haramu na usambazaji nyamapori katika eneo hilo hususan minadani.
Mfanyabiashara wa chakula maarufu kama mama lishe katika eneo hilo la Nkaiti, Tumaini Seuri anasema kwa muda wa miaka miwili sasa amekuwa akifanya biashara hiyo katika minada ya Minjingu na Mwada lakini hawajahi kununua wala kuuza nyamapori.
Aponea chupuchupu kwenda jela
Mmoja wa washukiwa wa biashara haramu ya nyamapori ambaye hakutaka jina lake liandikwe amekiri kukamatwa mwaka 2020 akiwa kwenye shughuli zake za upishi katika mnada wa Minjingu.
“Mimi sikujua kama Ile ilikuwa ni nyamapori kwa sababu sina huo utaalam, lakini kwa bahati nzuri aliyeniuzia nilikuwa namfahamu, niliwaonyesha askari na wakamkata, tena alikuwa bado anayo nyama nyingine kidogo mbichi.
“Kwa kweli nashukuru niliponea chupuchupu kufungwa, sitarudia tena na pia imenisaidia nimekuwa makini zaidi siku hizi na nyama,” anasema mama huyo.
Uuzaji nyamapori wadhibitiwa
Tumaini anakiri kuona mmoja wa mama lishe akitiwa nguvuni na askari wa wanyamapori kwa tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo.
“Toka nimezaliwa sijawahi kupelekwa polisi, ndo nije kushikwa na uzee huu, sitaki…hiyo biashara sijawahi kufanya, zamani kidogo niliwaona askari wakikamata watu lakini sikujua nini kimetokea zaidi kwake,” anasema.
Baada ya kushamiri kwa vitendo hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wameamua kuchukua hatua kwa kutoa elimu za uhifadhi kwa wananchi wanaoishi jirani na hifadhi ili kuzifanya kuwa endelevu.
Hatua hiyo ni pamoja na kuwepo kwa mifumo, sheria na kanuni kwa jamii iliyosaidia kuzuia na kulinda wanyamapori hususani twiga na swala ambao wamekuwa wakiwindwa zaidi katika ushoroba huo.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizoingia na kutekeleza Mkataba wa Lusaka wa kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyama na mimea ndani na nje ya bara hilo (Lusaka Agreement Task Force-LATF) ilianzishwa mwaka 1994.
Visa vya ujangili vinazidi kupungua mwaka hadi mwaka katika eneo la ushoroba huo ambapo Takwimu za Jumuiya ya Hifadhi ya wanyamapori ya Burunge (Juhibu) zinaonyesha kuwa ujangili umepungua karibu mara nane katika jumuiya hiyo kutoka visa nane mwaka 2021 hadi visa viwili mwaka 2023.
Unafuu wanukia
Hata katika ngazi ya Taifa vitendo vya ujangili wa wanyamapori vimepungua. Taarifa ya hali ya usalama iliyotolewa Juni 2023 na Wizara ya Maliasili na Utalii inabainisha kuwa katika kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Aprili 2023 hakuna vifo vya wanyamapori vilivyotokana na ujangili vilivyoripotiwa Tanzania.
Ujangili unaofanyika katika hifadhi ya Juhibu kwa kiwango kikubwa ni ujangili kwa ajili ya kitoweo huku baadhi ya wanawake wakitumika zaidi kwa kununua na kuuza nyamapori kinyume na sheria kupitia biashara ya mama lishe katika minada mbalimbali.
Sera ya wanyamapori ya Tanzania ya mwaka 2007 inaitaka serikali na wadau wa uhifadhi kulinda shoroba za wanyamapori, njia za uhamiaji, maeneo ya usalama wa wanyama na kuhakikisha kwamba jamii zilizo katika maeneo hayo ya wanyama zinafaidika vilivyo kutokana na uhifadhi wanyamapori bila kuvunja sheria za uhifadhi.
Uchunguzi wa awali umeonesha kuwa elimu juu ya madhara ya ujangili umechangia jamii kuelewa umuhimu wa uhifadhi. Katika kulinda wanyamapori hao, Serikali na wadau wameweka kikosi kazi cha askari wa wanyamapori wa Burunge WMA wapatao 40 kutoka taasisi nne za Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), shirika lisilo kuwa la Serikali la Chem Chem Association, Burunge WMA pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Babati.
Katibu wa Burunge WMA, Benson Mwaise amesema kwa kushirikiana na taasisi hizo nne wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja ya kutoa elimu kwa jamii juu ya uhifadhi wa maliasili, kufanya doria pamoja na kuhakikisha watuhumiwa wanapelekwa katika vyombo vya sheria.
“Watu wanaofanya biashara ya chakula maarufu kama mama n’tilie ni wadau wetu muhimu sana kwa sasa, wao mara nyingi ndiyo wanaotupa taarifa za uwepo wa nyamapori katika minada, au kutupa taarifa za sehemu fulani kuna nyama inauzwa au inaletwa kuuzwa mnadani,” amesema Mwaise.
Anasema elimu kwa wanawake imekuwa mkombozi dhidi ya ujangili na sehemu kubwa ya ulinzi wa wanyamapori na hii inatokana na hapo awali wanawake kutumika kama wanunuzi wakuu wa nyama hizo kutoka kwa majangili.
“Kwa kuwa mama lishe walikuwa hawajapata elimu ya uhifadhi, wao waliangalia faida wanayoipata kwani walikuwa wakiuziwa nyamapori kwa bei ndogo sana ikilinganishwa na nyama nyingine kama ya ngo’mbe, kondoo na mbuzi,” anasema Mwaise.
Uhifadhi wa Jumuiya hiyo ni shirikishi kwa kuwa umekuwa ukishirikisha kwa kina wanawake na vijana katika kulinda rasilimali hizo.
Vijiji vyajitosha uhifadhi
Mwenyekiti wa kijiji cha Vilimavitatu Aboubakar Msuya anaeleza kuwa nafasi ya kijiji chake ni kulinda na kuhakikisha kunakuwepo mazingira salama ya uhifadhi kwa kuzuia ujangili wa nyamapori.
“Hata minada iliyopo hapa kwenye kijiji chetu huwezi kukuta mama lishe wanapika ndani mnadani, hapa kwetu wanapikia majumbani mwao halafu wanapeleka kuuza chakula kilichokuwa tayari,” anasema Mwenyekiti huyo akibainisha kuwa si rahisi kukuta mtu anauza nyamapori kiholela.
Kupungua kwa ujangili katika ushoroba huo unathibishwa pia na Mwenyekiti wa Kijiji Cha Minjingu Samwel Melami ambaye anasema kijiji chke hakina ujangili wa wanyamapori kwa sababu hata asili ya wakazi wa eneo hilo ni jamii wa wamaasai ambao hawali nyamapori.
“Hapa tuna mtandao wa taarifa za siri hususani mnyama anapoonekana, hata kwenye mnada sijawahi kusikia kuna watu wamekamatwa na nyamapori, labda kama wanawakamata bila sisi viongozi wa kijiji kupewa taarifa,” anasema.
Daud Melengoli Mollel, Mwenyekiti wa Kijiji Cha Olasiti anasema “Sisi tunafahanu umuhimu na faida ya uhifadhi, kwa hiyo siyo rahisi wananchi kufanya ujangili, na hadi muda huu tunavyozungumza hatuna tukio lolote la ujangili katika Kijiji chetu.”
Diwani wa Kata ya Nkaiti, Steven Sarun Mollel anasema kabla ya kuundwa kwa Burunge WMA miaka 18 iliyopita kulikuwa na matukio mengi ya ujangili kwa sababu wanyama walikuwa wanazagaa vijijini hivyo waliuawa kiurahisi, lakini baada ya kuanzishwa Kwa jumuiya hiyo wanyama wamepita njia sahihi ya mapitio.
Elimu, doria ni muarobaini wa ujangili
Afisa Tawala Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili kutoka Chem Chem Association, Ernest Elia anasema wao hufanya kazi kubwa mbili ambazo ni kuweka ulinzi na kufanya ufuatiliaji kupitia kikosi cha doria cha pamoja.
Amesema lengo la uwekezaji huo ni kupunguza utegemezi wa jamii kwenye maliasili katika kujiingizia kipato na kubuni biashara mbadala ambayo ni rafiki wa uhifadhi jambo ambalo limesaidia kupunguza ujangili kwa kiasi kikubwa.
Ili kuonyesha kuwa Serikali imedhamiria kumaliza tatizo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Tangwe amesema kupitia vikao vya mara kwa mara vya ujirani mwema na vijiji vilivyozunguka uhifadhi wamefanikiwa kupunguza ujangili.
Katika kuhakikisha kuwa ushoroba huu unakuwa endelevu, mwaka 2009 serikali iliunda Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambayo ilianza kazi rasmi mwaka 2016.
Kwa mujibu wa TAWA hadi kufikia mwezi Aprili 2023 katika mwaka wa 2022/2023, jumla ya doria 195,912 sawa na asilimia 69 ya lengo la siku doria 284,460 zimefanyika nchini.
Doria hizo zimefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa 2,786; bunduki 108; risasi 1,334; kutegua mitego 3,080 ya nyaya za kutegea wanyamapori.
Ripoti hii maalumu ni sehemu ya mafunzo ya uandishi wa habari za bioanuai yaliyofadhiliwa na Watu wa Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili na kuratibiwa na Nukta Africa.