Egidia Vedasto
APC Media
Vijana wametakiwa kuikataa elimu yenye chembechembe za kikoloni inayodumaza akili zao na kuwafanya kukosa uwezo wa kubuni na kuchanganua mambo katika mifumo chanya.
Hayo yameelezwa na Rais wa Asasi zisizo za Kiserikali nchini (AZAKI), Dkt. Stigmata Tenga ambaye amewataka vijana kubadilika na kuanza kujiingiza kwenye michakato ya kushiriki kutunga Sheria na kutokukubali kuwa wategemezi wa fikra bali kujitegemea na kufanya maamuzi sahihi yatakayobadilisha taswira ya maisha yao.
“Katika Dira ya Taifa ya 2050 na Tanzania tuitakayo lazima vijana waamke na wawe wabunifu, kwani Serikali inatengeneza Sera kwa ajili yenu Vijana na Watoto, na nyie ndio wajenzi wa taifa la kesho” ameeleza Dkt. Tenga.
Kwa upande wake aliyekuwa Mgeni rasmi katika ufunguzi wa wiki ya AZAKI Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, ameipongeza AZAKI kwa jitihada zake kubwa na ushirikiano wa kina na Serikali katika uboreshaji wa huduma za jamii na kuinua uchumi wa wananchi.
Aidha prof. Mkumbo ameongeza kwamba, Serikali inaendelea kupambana kuleta maendeleo kwa wananchi ili ifikapo 2050 kusiwe na mwananchi fukara, asilimia 60 ya wananchi wawe ni wanaojua kusoma na kuandika na uhakika wa umeme kuvutia uwekezaji.
“Naiona Tanzania ijayo kuwa ya haki kwa kila mtu, shindani na yenye watu wenye maarifa ya kwenda popote duniani na serikali yenye uwezo na nguvu ya kutosha ya kufanya maamuzi ili kutengeneza jamii yenye fikra chanya” amesema Prof. Mkumbo.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa AZAKI Justice Rutenge amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuletea wananchi maendeleo na kuwataka wajitambue na kujitetea vile wanataka waendeshwe.
“” Tunataka kuvuka vikwazo katika sekta ya elimu, afya, kilimo, utawala bora na nyingine nyingi” ameeleza Rutenge.
Mmoja wa washiriki katika Wiki ya AZAKI Mkurugenzi wa Taasisi ya Usawa wa Ukuaji iliyopo Dar es salaam,Jane Magigita amesema wanataka kubadilisha mfumo wa mawazo hasi unaobadilisha maono kuwa ya kikoloni hali inayotishia watu wengi na kudumaza maendeleo yao.
Ameongeza kwamba, kuna umuhimu wa kushirikiana na makampuni makubwa na viwanda vikubwa ili kwa pamoja kuweza kubadilisha maisha ya wananchi.
“Msisitizo wa Tanzania tuitakayo na lengo la serikali ni kila Mtanzania kuishi maisha mazuri yenye ustawi huku tukichagiza jitihada za serikali katika kuleta maendeleo na mabadilko kwa watu wa makundi maalum” ameeleza Magigita.