Wakulima wa parachichi njombe wapewa somo kupata mazao bora

 Na Joctan Myefu , Njombe 

WASIMAMIZI (Farm Managers) 70 kutoka kampuni tofauti za mashamba ya parachichi yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 900 mkoani Njombe wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kufanya kilimo hai ili kuweza kuzalisha kisasa na kupata mazao mengi zaidi.

Mafunzo hayo yaliyotolewa na  kampuni ya Guavay pia yalilenga kuwajengea uwezo maafisa hao kuweza kuongeza thamani na ubora utakaokuwa na ushindani katika soko la ndani na nje ya Tanzania.

Licha ya takwimu kuonyesha kuwa Tanzania inazalisha zaidi ya Tani elfu 8 hadi 9 kwa mwaka na Kenya kuzalisha tani elfu 90 kwa mwaka lbado malighafi inayozalishwa nchini bado imekuwa na changamoto sokoni kwa kuwa wakulima wengine wamekuwa wakitumia kemikali katika kilimo hatua ambayo inatajwa kuwa na athari kwa walaji na kulazimika kupendelea mazao ya oganiki.

Mkurugenzi wa kampuni ya Guavay, Ahadi Katela amesema kampuni yake imelazimika kutoa elimu hiyo ya kilimo hai kwa wakulima ili kutengeneza soko la uhakika ndani na nje ya Tanzania na kuwawezesha wakulima wa Tanzania kiuchumi zaidi.

Christina Myonga msimamizi wa shamba la shule ya sekondari Mtwango na Yohanes Nyawike  ni baadhi ya wanufaika wa mafunzo ya kilimo hai ambao wanasema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakipata mazao duni kutokana na kutozingatia taratibu za kilimo hicho na kwamba elimu hiyo inawafanya kwenda kufanya mapinduzi huku pia wakiomba wataalam wa serikali na taasisi za kilimo kuendelea kuwatembelea na kuwaelimisha.

Nae muwezeshaji wa mafunzo hayo Musa Joshua amesema mbali na kutoa elimu kwa wasimamizi lakini amewashauri wawekezaji wakubwa na wadogo kuhakikisha wanaweka mazingira bora na rafiki kwa mnunuzi na mfanyakazi ili kuongeza hamasa kwa wengine .

Wakulima wakiwa katika mafunzo 

Mkurugenzi wa kampuni ya Guavay, Ahadi Katela