Waziri mkuu: fedha za ndani zijenge miradi ya kimkakati

WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya
Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga wahakikishe wanajenga mradi wa
kimkakati kwa kutumia fedha za mapato ya ndani na si kusubiri miradi
kutoka Serikali Kuu wakati wanakusanya zaidi ya sh. bilioni saba kwa
mwaka.


Amesema
halmashauri hizo licha ya kukusanya fedha nyingi kwa mwaka lakini
matumizi yake si mazuri kwa sababu hawana mradi wowote wa kimkakati
wanaoutekeleza, mfano ujenzi wa maeneo ya kuegeshea magari makubwa au
hata ujenzi wa kituo cha mabasi, miradi ambayo ingewaongezea mapato.

Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Septemba 26, 2019) wakati
akihutubia na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
uwanja wa Wambi wilayani Mufindi akiwa katika ziara yake ya kikazi
mkoani Iringa.”Nataka kuona mradi wa kimkakati ukitekelezwa kwa fedha
mnazokusanya kutoka kwa wananchi.”

Alisema
viongozi hao wanaweza kutenga kiasi cha sh. bilioni moja kwa mwaka na
kujenga hospitali au wakatenga fedha na kujenga barabara za lami kwa
awamu katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa kuwa ujenzi wa barabara
za lami mijini ni sh. milioni 300 kwa kilomita moja, hivyo wangeweza
kutekeleza ujenzi huyo kutokana na fedha wanazokusanya.

“Msitegemee
fedha kutoka Serikali Kuu tu jengeni wenyewe barabara zenu kuzunguka
Mji wa Mafinga kwa kiwango cha lami kwa sababu mna fedha za kutosha tena
mnaweza kutumia fedha za mapato ya ndani mnazokusanya kutoka kwa
wananchi badala ya kuzitumia kwa kulipana posho tu.”

Awali,Waziri
Mkuu alitembelea shule ya Sekondari ya kata ya Mdabulo na kupokea
taarifa fupi ya ujenzi wa bwalo, bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike
pamoja na ujenzi wa madarasa na kisha alizungumza na wananchi na
kuwaeleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwenye maeneo
yao.

Waziri
Mkuu alisema katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya
karibu na maeneo yao ya makazi, Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa
vituo vya afya katika kila kata pamoja na ujenzi wa hospitali za wilaya
ikiwemo na wilaya yao ya Mufindi ambayo ipo katika hatua mwisho
kukamilika.

Kwa
upande wao, wabunge wa mkoa wa Iringa wakiwemo wa majimbo na wa viti
Maalumu kwa nyakati tofauti waliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kutoa fedha za ujenzi wa
miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye mkoa wao.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,