Na Mwandishi Wetu, Arusha
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Arusha imekiri kupokea malalamiko ya rushwa dhidi ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo,na kwamba inaendelea kuchunguza malalamiko hayo yanayohusiana na kura za maoni za kumpata mgombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya CCM zilizofanyika Julai 20, mwaka huu.
Kwa mujibu wa TAKUKURU, Gambo ambaye aliibuka mshindi katika kura hizo kwa kupata kura 333 kati ya 478, ni miongoni mwa wagombea 20 ambao walilalamikiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa kabla na siku ya upigaji wa kura hizo.
|
Kaimu Kamanda wa Takukuru mkoani humo James Ruge amemtaja mfanyabiashara wa jijini hapa, Philemon Mollel (MONABAN),kuwa kati ya wagombea hao 20 wanaolalamikiwa,na kuwa ameshahojiwa mara mbili na simu zake zinashikiliwa na taasisi hiyo kwa uchunguzi zaidi. Monaban aliibuka mshindi wa pili katika kura hizo za maoni baada ya kupata kura 68.
“Tumepokea malalamiko mengi ya rushwa katika kura za maoni za CCM, tumewahoji baadhi ya watuhumiwa na tunaendelea.Tukimaliza uchunguzi, tutawataarifu,” amesisitiza Kaimu Kamanda huyo.
Alipobanwa kuhusu Gambo, Ruge ambaye mwanzoni alionekana wazi kumsafisha mkuu huyo wa zamani mkoa,kwa kudai kuwa hajawahi kuoijiwa na taasisi hiyo,amekiri kuwa malalamiko mengi dhidi yake (Gambo) yamefikishwa ofisini hapo na yanashughulikiwa kama ilivyo kwa watuhumiwa wengine.
Upigaji kura za maoni hasa katika Jimbo la Arusha Mjini umezua malalamiko mengi ya rushwa kutawala kiasi cha kusababisha wagombea Tisa Kati ya 90 kuandika barua za malalamiko kupinga mchakato mzima.
Baadhi ya tuhuma zinazoelekezwa kwa Gambo na kambi yake ni pamoja na kutoa fedha kuanzia sh150,000 hadi 200,000 kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa kura za maoni.