Mhasibu wa wizara ya afya kortini kwa mashitaka 280

Mhasibu
wa Wizara ya Afya, Luis Lyimo (54) na Mtendaji Mkuu wa taasisi ya
Christian Social Services Commission, Peter Maduki (61) wamefikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na
mashtaka 280 yakiwemo 150 ya kughushi na moja la kutakatisha fedha.


Mawakili
wa Serikali , Zakaria Ndaskoi na Genes Tesha wamewasomea mashtaka
washtakiwa hao jana  Jumatatu Januari 6, 2020 huku wakipokezana mbele ya
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando.

 
Wakili Ndaskoi amedai washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya mwaka 2017 na mwaka 2019 ndani ya Jiji la Dar es Salaam

Alidai
washtakiwa hao kwa nafasi zao wakiwa na nia ovu walighushi hundi
mbalimbali zenye thamani ya mamilioni ya fedha na kusaini kwa jina la
Upendo Mwingira bila ridhaa yake huku wakijaribu kuonyesha mshtakiwa,
Luis Lymo alikuwa akilipwa na taasisi ya Christian Social Services
Commission Fedha hizo kama kamisheni wakati si kweli.

Katika
mashtaka ya kuwasilisha nyaraka za uongo washtakiwa hao wanadaiwa
kuwasilisha nyaraka mbalimbali walizozighushi katika benki ya Standard
Chartered.

Baada
ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongeza
chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikilizwa kesi ya
uhujumu uchumi.

Upande
wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika, washtakiwa walipelekwa
rumande na kesi imeahirishwa mpaka Januari 20 2020

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *