Takukuru kumpandisha kizimbani hakimu kwa tuhuma ya kupokea rushwa

Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein Mzee Mussa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) Mkoani Shinyanga inatarajia kumfikisha Mahakamani Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Kishapu Benjamin Charles Mhangwa kwa tuhuma
za kuomba na kupokea rushwa kinyume cha kifungu cha 15 cha sheria ya
kuzuia na kupambana na rushwa Na 11 ya Mwaka 2007.


Akizungumza na waandishi wa habari leo
Jumatano Oktoba 9,2019 Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein
Mzee Mussa amesema hakimu huyo aliomba na kupokea kiasi cha shilingi
200,000 kati ya shilingi 300,000/= alizoomba kutoka kwa Juma Mbugi kuwa
ametumwa na hakimu wa wilaya ya Kishapu Wilberforce Luwago ili kusaidia
kupata ushindi katika kesi ya kubakwa kwa mwanawe.

Aidha kwa mujibu wa uchunguzi
uliofanyika umebaini kuwa fedha hizo hazikuombwa na hakimu Mkazi
Mfawidhi wa wilaya ya Kishapu Wilberforce Luwago hivyo mtuhumiwa huyo
aliomba na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.