Wafungwa 136 waachiwa huru simiyu kufuatia msamaha wa rais, waahidi kuwa raia wema

Na Stella Kalinga, Simiyu

Jumla
ya wafungwa 136 kutoka magereza za Mkoa wa Simiyu wamechiwa huru
kufuatia msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
John  Pombe  Magufuli alioutoka Desemba, 2019 katika sherehe za
maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika jijini
Mwanza.



Akitoa
taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari Desemba 10, 2019 Mkuu wa
Jeshi la Magereza Mkoa wa Simiyu, ACP. Andulile Mwasampeta amesema 
anamshukuru Mhe. Rais Magufuli  kitendo hicho cha kutoa msamaha ambacho
kimesaidia kupunguza msongamano kwenye magereza ya mkoa wa Simiyu.

“Ninamshukuru
sana Mhe. Rais Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa
kutoa msamaha huu ambao umepunguza msongamano katika magereza yetu
hususani gereza la Bariadi; nitumie nafasi kuwaasa wafungwa
waliosamehewa kwenda kuwa raia wema na wakafanye kazi halali na
wasifanye makosa yatakayowaleta tena hapa gerezani,” alisema ACP
Mwasampeta

ACP
Mwasampeta ameongeza kuwa wafungwa 136 waliopata msamaha wa Rais katika
mkoa wa Simiyu ni wale waliokuwa wamebakisha muda wa  siku moja hadi
miezi sita miezi 12 kumaliza muda wa vifungo vyao, ambapo amebainisha
kuwa wamezingatia maelekezo ya Mhe. Rais katika vigezo vya watu
walioachiwa huru.

Aidha,
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa kufanikisha zoezi la
kuwaleta pamoja wafungwa wote waliopata msamaha wa  Rais kwa kutoa
magari  yaliyowezesha jeshi la magereza kuwachukua katika magereza
mbalimbali mkoani Simiyu na kuwaleta katika gereza la Bariadi ambapo
ndipo walipoanzia safari ya kurejea majumbani kwao.

Kwa
upande wao wafungwa waliopata msamaha wa Rais na kuachiwa huru
wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa msamaha huo na kuahidi kuwa
raia wema watakaofanya kazi halali na kujiepusha na makosa yote
yanayoweza kusababisha wakarudi tena gerezani.

“Namshukuru
sana Mhe. Rais kwa msamaha huu alioutoa kwa wafungwa zaidi ya 5000
tuliokuwa magereza mbalimbali niseme tu kwamba wale wote waliokuwa
wafungwa kama mimi na wakapata msamaha huu tukawe raia wema na tukachape
kazi tujenge nchi yetu, “ alisema Buluba George miongoni mwa wafungwa
136 mkoani Simiyu

“Mimi
naahidi kwenda kujishughulisha na shughuli za kuniwezesha kupata
kipato, nitajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili nisije nikaletwa tena
huku gerezani, namshukuru sana Rais Magufuli kwa kutupa msamaha huu,”
alisema Musa Lazaro miongoni mwa wafungwa 136 mkoani Simiyu