Na Egidia Vedasto
Arusha
Serikali imeweka mazingira rafiki na thabiti kwa makundi yote katika jamii kufikiwa katika ukusanyaji maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa maana ya kutoa maoni na mapendekezo ya namna gani nchi iendeshwe.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Arusha, Mmoja wa Waandidhi wa Dira hiyo Mwanazuoni na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Idara ya Saikolojia Dr. Richard Shukia amesema ni vema wananchi waendelee kutoa maoni kwa wingi kwani Dira ya Taifa ya Maendeleo ni Wananchi siyo ya Serikali.
Aidha amepongeza idadi kubwa vijana wanaoendelea kutoa maoni yao huku akisisitiza kundi la wanawake kutambua umuhimu wa kutoa maoni yao na kudumisha amani na utulivu wa nchi.
“Kwa Makundi maalum ya Watu wenye ulemavu, tunazingatia miundombinu rafiki ili wawasilishe maoni yao kwa ufasaha na kwa wakati” amesema Dr. Shukia.
Sambamba na hayo amebainisha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kutokana na Dira iliyopita ambayo ni katika nyanja za afya, elimu, Mawasiliano na Miundombinu.
“Ukiachana na mafanikio hayo lakini pia kuna changamoto ambazo zinachangia kutokufikia kwa malengo ya Dira ya maendeleo ikiwemo mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo husababisha mafuriko ukame, maporomoko na maafa mengine, na mlipuko wa ugonjwa wa COVID uliochangia idadi kubwa ya watu kukosa kazi kwa wakati huo” amefafanua Dr. Shukia.
Hata hivyo kesho kutakuwa na mkutano wa makundi mbalimbali ya wananchi katika ukumbi wa AICC jijini Arusha utakaowapa nafasi ya kujadiliana na kutoa maoni jinsi wanataka nchi iendeshwe na kuingia katika ujamaa na kujitegemea.
Kwa upande wake Mwandishi wa Redio Five Ashura Mohamed ametoa maoni yake juu ya maandalizi ya dira mpya ya 2050 kwamba, ni muhimu wanawake na vijana waone umuhimu wa kutoa maoni yao ili Serikali itambue nini kiongezwe na nini hakiko sawa katika suala la huduma za kijamii.
“Leo sisi ni vijana lakini miaka 25 ijayo tutakuwa wazee, hivyo tutoe maoni chanya yatakayoijenga Serikali yetu na kutupa huduma bora” amesema Ashura.
Katika namna hiyo hiyo Mwandishi wa Habari wa Redio Safina iliyopo Jijini Arusha Willy Cosmas amesema semina aliyoipata imempa hamasa ya kutambua umuhimu wa kutoa maoni na kuhamasisha vijana wengine na jamii kwa ujumla kutoa maoni sawasawa na inavyotakiwa kama haki yao ya msingi.
“Nitaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali juu ya fulsa hii muhimu ili tupate Dira nzuri 2050 itakayotupa nafasi ya kuzidi kukuza uchumi wetu kama Taifa” ameeleza Willy.