Waziri kigwangalla aaigiza maboresho ya huduma mlima kilimanjaro

Na Aron Msigwa – WMU, ARUSHA.

Waziri
wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla ameliagiza Shirika la
Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA) lifanye maboresho ya miundombinu ya
huduma za dharula na uokoaji ndani ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro ili
kuongeza usalama wa watalii wanaokweda kupanda mlima huo.


Pia,
amelitaka shirika hilo liendelee kuboresha miudombinu ya malazi katika
hifadhi hiyo ili iweze kuendana na mahitaji ya sasa ya wapanda mlima na
kuangalia uwezekano wa kutafuta wawekezaji watakaojenga hoteli za kisasa
kwa lengo la kuvutia watalii wengi zaidi.

Dkt.Kigwangalla
ametoa maagizo hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya
TANAPA na Wakuu wa Kanda wa Shirika hilo jijiini Arusha.

Amesema
hatua hiyo imekuja kufuatia changamoto mbalimbali alizokutana nazo
wakati akipada mlima Kilimanjaro Septemba, 28 mwaka huu, akiwa
ameambatana na kundi la Wasanii na wadau mbalimbali kutoka taasisi za
umma na binafsi.

Dkt.
Kigwangalla ameieleza Menejimenti hiyo kuwa katika zoezi lake la
kupanda mlima Kilimanjaro kuna changamoto alizibaini zikiwemo za
kukosekana kwa miudombinu ya kutosha ya huduma za uokoaji na malazi
ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka ili kuongeza ufanisi na
idadi ya watalii wanaopanda mlima huo.

Kufuatia
hali hiyo ameiagiza TANAPA ianze kuboresha huduma za dharula na uokoaji
pia ijenge vituo vya kutolea tiba na huduma ya kwanza mlimani
vitakavyokuwa na wataalam wa kuhudumia watalii wanaopata matatizo wakiwa
mlimani pia kuboresha huduma za malazi katika baadhi njia za mlima huo.

Dkt.Kigwangalla
amesema changamoto hizo zikitatuliwa kwa haraka zitauwezesha mlima huo
kupata idadi kubwa ya watalii kuliko ilivyo sasa na kuiogezea serikali
mapato.

Kuhusu
uboreshaji wa huduma za uokoaji (Rescue services) kwa watalii
wanaopanda mlima Kilimanjaro ameiagiza TANAPA ifanye utaratibu wa
kuazisha huduma ya viberege maalum (Zip line) vitakavyokua vinatumika
kushusha wapada mlima watakaokua wakipata matatizo ya kiafya kwa haraka
hata wakati wa hali mbaya ya hewa.

“Suala
la matumizi ya “Zip line” mliongezee nguvu ya kulitekeleza, hii itakua
njia rahisi ya uokoaji na itawajengea ujasiri wapada mlima waelewe
kwamba hata kama watapata shida yoyote ya kiafya wakati wa kupanda mlima
wanajua wana uhakika wa usalama wa maisha yao hata pale ambapo hali ya
hewa ni mbaya na helikopta haiwezi kutua mlimani” Amesisitiza Dkt.
Kigwangalla.

Amesema
uwepo wa huduma hiyo ya kisasa ya kushusha watalii wanaopata chagamoto
za kiafya itawezesha watalii kupata huduma mlimani kupitia vituo vya
kutolea huduma ya kwanza vitakavyojegwa mlimani ambavyo vitakua na
wataalam wenye mafumzo watakaokuwa na jukumu la kutoa huduma muda wote.

Kuhusu
uboreshaji wa huduma ya malazi mlimani Dkt. Kigwangalla ameonesha
kuridhishwa na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na TANAPA kuboresha
miundombinu ya malazi mlimani na kuitaka iangalie uwezekano wa 
kuhamasisha wawekezaji wakubwa kwenye ujenzi wa hoteli za kisasa. 

Amesema
uwepo wa hoteli hizo pamoja na mambo mengine utaongeza siku za watalii
kukaa mlimani akitoa mfano wa hoteli nzuri na za kisasa zilizojengwa
katika milima ya Alaps ambazo zinatembelewa na watu maarufu kutoka
maeneo mbalimbali duniani.

Kufuatia
maagizo hayo, Kamishna wa uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA), Dkt. Allan Kijazi amesema kuwa TANAPA inaendelea kufanya
maboresho kwenye maeneo ya kulala wageni ili yaweze kwenda na wakati pia
yawe na uwezo wa kupokea wageni wengi pia kuishirikisha sekta binafsi
katika utoaji wa huduma mlimani.

Amesema
kazi ya kuainisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa hoteli za kisasa
inaendelea na kwa kuanzia maeneo manne yamekwishaainishwa kwa ajili ya
uwekezaji na kuongeza kuwa baadhi ya wawekezaji wamekwishajitokeza na
kuonesha nia ya kujenga hoteli za kisasa katika mlima huo.

Kuhusu
uboreshaji wa huduma za ukoaji mlimani amesema kwa sasa kuna maeneo
yana miundombinu ya barabara zinazowezwsha magari ya kubebea wagonjwa
kufika katika baadhi ya maeneo na kutoa huduma ya uokoaji.

 Pia
amesema wamekua wakitumia helikopta kutoa huduma za uokoaji licha ya
huduma hiyo kushindwa kufanyika kazi wakati wa hali mbaya ya hewa na
hivyo kulazimika kutumia machela za matairi zinazoendeshwa na watu
kuhudumia watalii wanaopata matatizo ya kiafya.

Aidha,
Dkt. Kijazi amesema TANAPA inaendelea kufanya maboresho ya huduma za
dharula na uokoaji na itawasilisha kwake taarifa ya utekelezaji
itakayoainisha mpango wa ujenzi wa njia za kisasa zitakazotumia
viberenge maalum vya uokoaji vitakavyokua vikipita kwenye waya (Zip
line) ili kazi ya ujenzi wa njia hizo ianze mara moja.